Network blog

Teknolojia ya Blockchain na Sarafu Zinazoshirikisha Jamii katika Misaada ya Kibinadamu Nchini Kenya

Na Rosemary Okello-Orlale (Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Strathmore) na Steve Kenei (Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya), tarehe 2 Juni 2021. [The original English blog post is available here]

Majanga na hali ya mizozo mara nyingi huambatana na matukio ya kuhama kwa watu wengi barani Afrika. Mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara yana kambi nne kati ya kambi za wakimbizi zilizo kubwa zaidi duniani. Wakimbizi wengi katika kambi zilizo nchini Kenya, hasa katika kambi za Kakuma na Dadaab, wamekuwa wakipata misaada kwa njia za zamani. Katika kambi hizi, mara nyingi misaada huja kwa namna ya usaidizi wa pesa taslimu, kupitia malipo ya mara kwa mara au miradi ya kulipwa kwa kufanya kazi. Hii inaendana na mabadiliko mapana katika utoaji wa misaada ya kibinadamu yanayoelekea usaidizi wa kutoa pesa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la utumiaji wa fedha dijitali kwa njia ya simu. Katika mkutano wa Ngazi ya Juu ulioandaliwa na Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Strathmore (SBS) kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (KRCS) na Kituo cha Kimataifa cha Masuala ya Kibinadamu (International Centre for Humanitarian Affairs) mwaka 2018, ilibainika kuwa katika mazingira yanayobadilika kila wakati ya misaada ya kibinadamu, ni mambo machache sana hubaki yalivyo na kwamba pana haja kwa mashirika ya kibinadamu kutafuta njia bunifu za kutoa misaada kwa ubora na ufanisi huku yakiendelea kuwa na uthabiti wa kifedha. Wakati wa mkutano huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, Dkt. Abbas Gullet, aliangazia changamoto muhimu zinazohusiana na miundomsingi ya kiuchumi kwa jamii zilizotengwa katika kambi hizi na kwamba kiasi kikubwa cha misaada ya pesa inayotolewa na mashirika ya kibinadamu hutoka haraka sana nje ya jamii hizo na hivyo kutokuwa na athari ya kudumu. Aliongeza kwamba watu walio muhimu katika jamii, mitandao na rasilimali za jamii hizo bado hazitumiwi kikamilifu. Alizungumza kuhusu utumiaji wa teknolojia ya blockchain katika sekta ya misaada ya kibinadamu, huku akitoa mifano kutoka kwa wadau ambao wametumia au kuanzisha mifumo ya blockchain katika kazi zao.

Picha kwa hisani ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Nairobi)

Jamii zilizo katika hatari ya kuathirika hazikosi mawazo ya kuboresha hali zao wenyewe. Yamkini wanachohitaji ni chombo bora cha kubadilishana bidhaa na huduma kinachowawezesha kutumia rasilimali zao ambazo hazitumiwi kikamilifu, pamoja na kuzalisha mtaji wa kifedha wenyewe ndani ya jamii. Kwa mtazamo wa mashirika ya misaada ya kibinadamu, pia kuna wasiwasi unaohusiana na uwajibikiaji wa misaada ya pesa ambayo wanatoa – wasiwasi huo unahusu jinsi wanavyoweza kuhakikisha kuwa pesa wanazotoa zinatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa, kwamba zinakidhi mahitaji ya vikundi vilivyo hatarini zaidi, na kwamba pesa hizo zinabaki katika jamii lengwa. Mahitaji haya yameleta haja ya kukuza vyombo vipya vya kubadilishana bidhaa na huduma, ambavyo vinaweza kuoanisha ujumuishwaji wa kifedha wa watu waliotengwa na uadilifu wa kifedha pamoja na uwajibikaji wanaouhitaji wafadhili. Teknolojia zinazoibuka kama vile blockchain zinaonekana kutoa fursa zinazohusiana na mahitaji haya, na ndizo msingi wa kubuniwa kwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii (Community Inclusion Currencies – CIC). Chapisho hili la blogu linafafanua Sarafu Zinazoshirikisha Jamii zinazotegemea teknolojia ya blockchain, zinavyofanya kazi, jinsi na kwa nini zinajaribiwa katika Kaunti za Nairobi na Mombasa nchini Kenya. Pia tumezingatia hoja kadhaa muhimu ambazo zinatokana na ukuaji na utumiaji wa teknolojia kama hizo, tukizingatia ulinganifu unaofaa kuwepo kati ya kudumisha faragha na uhuru wa wanaopokea misaada, na mahitaji ya mashirika ya misaada ya kupata uwajibikaji na kuhakikisha kuwa misaada inatimiza malengo yaliyokusudiwa.

Je, Sarafu Zinazoshirikisha Jamii kwa kutegemea teknolojia ya Blockchain ni nini?

Blockchain ni daftari dijitali la miamala. Kila muamala unaoongezwa kwenye blockchain huthibitishwa kwenye kompyuta kadhaa zilizo kwenye Intaneti na rekodi hii ya umma haiwezi kuvurugwa. Teknolojia ya blockchain ilibuniwa ili kuwezesha uwekaji hesabu wa sarafu dijitali ya Bitcoin, lakini imekua na sasa inawezesha aina nyingine za utunzaji wa rekodi kati ya wahusika binafsi. Sawa na tasnia nyingine, sekta ya misaada ya kibinadamu ulimwenguni imekuwa ikijihusisha kikamilifu katika kujaribu uwezo unaotokana na kutumia teknolojia ya blockchain katika shughuli zake, kwa mfano, katika usimamizi wa rekodi za miamala kwa uwazi ili kuondoa ufisadi au kuhimili mifumo ya utambulisho kwa watu wasio na aina nyingine za hati za kijitambulisha. Mashirika ya misaada ya kibinadamu pia yameanza kutumia teknolojia ya blockchain kubuni aina mpya ya fedha kwa ajili ya misaada. Fedha hizo zinaitwa, Sarafu Zinazoshirikisha Jamii.

Picha kwa hisani ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Nairobi)

Mojawapo ya miradi ya Sarafu Zinazoshirikisha Jamii iliyozinduliwa nchini Kenya katika miaka iliyopita kwa msaada wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya inaitwa Sarafu, ambayo ni vocha dijitali inayotegemea blockchain ya Ethereum. Wanajamii huitumia kununua na kuuza bidhaa za msingi katika mazingira ambapo sarafu ya kitaifa ni nadra. Vocha dijitali za Sarafu zinadhaminiwa na bidhaa na huduma zilizo katika jamii husika. Thamani ya vocha hizo katika eneo husika zinalinganishwa kwa namna inayokaribiana na sarafu ya kitaifa, kwa hivyo kiwango ambacho wauzaji wanaweza kubadilisha sarafu za CIC na sarafu za kitaifa kinategemea kiasi cha hazina au fedha za “mtaji” zinazosalia. Ingawa sarafu za CIC zilizo kwenye mzunguko katika jamii huwa na thamani ya 1:1 na sarafu ya kitaifa, jumla ya thamani inayoweza kubadilishwa kwa sarafu za kitaifa haiwezi kuwa zaidi ya thamani ya hazina ya sarafu hizo. Kwa upande wa wanaopokea, wanajamii husajiliwa na kupewa tokeni/Sarafu 400 ambayo ni sawa na Ksh 400 ili waweze kununua na kuuza bidhaa za msingi kama vile sabuni, maji na vyakula ndani ya jamii kutoka kwa wauzaji waliosajiliwa.

Chini ya mradi huo ulioitwa,  Kubadilisha Jamii Kupitia Vocha Dijitali za Blockchain, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (KRCS) lilianzisha utumiaji wa CIC ya Sarafu katika jamii mwezi Mei 2020 katika Kaunti za Nairobi na Mombasa. Mradi huu unasaidiwa na Ethereum Foundation – na unatumia mfumo huria wa Ethereum blockchain. Vilevile unahusisha ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la DenmarkIFRC na shirika la Grassroots Economics Foundation. Ingawa bado ni mradi wa jaribio, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii zinaweza kuigwa na kutumiwa katika miradi ya kupunguza umaskini katika jamii nchini Kenya na kwingineko. Haya yalinakiliwa katika mfululizo wa machapisho ya blogu yaliyoandikwa na Grassroots ambao walikuwa watoa huduma katika mradi huu.

Je, ni kwa nini mifumo iliyopo ya fedha dijitali isitumike (pesa kwa njia ya simu)?

Kenya imekuwa ikiongoza duniani katika kubuni mifumo ya miamala ya kifedha kupitia SMS na mfumo wa Safaricom wa  M-Pesa unatumika sana kote nchini. Nchini Kenya na kwingineko, mifumo kama hiyo ya kuhamisha pesa kupitia simu (ambayo haitumii teknolojia ya blockchain) pia hutumiwa kusambaza misaada ya kibinadamu. Hili linaibua swali: kuna haja gani kwa mashirika ya kibinadamu kuanzisha sarafu mpya za CIC zinazotegemea blockchain, badala ya kutumia miundomsingi iliyopo na inayotumika sana ya pesa dijitali? Kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu, suala kuu linahusu ni kipi msaada unaweza (au hauwezi) kutumiwa kufanya. Tofauti na mfumo wa pesa kupitia SMS, sarafu za CIC zinaweza tu kutumiwa na wapokeaji kununua aina fulani za bidhaa za msingi katika jamii wanamoishi. Kwa kufanya hivyo wafadhili wanalenga kupata usawa kati ya kuwapa walengwa uhuru mkubwa wa matumizi (ikilinganishwa na kuwasambazia vyakula au vitu visivyo vyakula) na wakati huo huo wakijaribu kuhakikisha kuwa misaada inatumiwa kwa vitu muhimu, na kwamba haitoki nje ya jamii lengwa. Kwa hivyo, mashirika hayo yanaamini kuwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii (CIC) huanzisha utaratibu unaoweza kuigwa katika jamii na kuna uwezekano utaratibu huo unaweza kuondoa umasikini kwa kujenga uchumi wenye mshikamano na endelevu katika maeneo husika. Inatarajiwa kuwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii zitakuza mahitaji na masoko ya maeneo husika na hivyo kufaidi jamii za wenyeji. Hili pia linaweza kupunguza uwezekano wa mizozo kati ya wenyeji na wakimbizi, kwa sababu wafanyabiashara wa eneo husika wakitumia Sarafu Zinazoshirikisha Jamii, kunaweza kuwa na faida kwa jamii pana ya eneo hilo. Kwa mashirika kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, mbali na kuwapa usalama wafanyakazi, Sarafu Zinazoshirikisha Jamii pia huyapa uwezo wa kuchanganua, kwa wakati halisi, mtiririko wa jumla ya sarafu iliyo katika jamii, jambo ambalo linaweza kusaidia shirika kubuni njia mbalimbali na stahimilivu za miunganisho ya kifedha miongoni mwa wenyeji.

Picha kwa hisani ya Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Nairobi)

Miradi kama hiyo inakusudia kusanifu upya mipango ya uhamishaji wa fedha ili iwe kichocheo kwa jamii kukuza na kufanya biashara zikitumia mbinu zao za ubadilishaji, ambayo ni msingi wa uchumi thabiti na jumuishi ndani ya kambi miongoni mwa wakimbizi. Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, Sarafu inawaruhusu wanajamii kufanya biashara miongoni mwao wenyewe na hivyo kuongeza tija, kukuza desturi ya kuweka akiba na kuwawezesha wanajamii waliosajiliwa kumudu mahitaji ya kimsingi.  Takriban kwa mwezi, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilishuhudia miamala yenye thamani ya Dola 95,600 za Marekani kwenye mtandao wa Sarafu, huku kukiwa na miamala 22,702 iliyotokana na watumiaji 2,588 ambao walisambaziwa tokeni 12,700 za Sarafu Zinazoshirikisha Jamii. Majaribio yanayoendelea nchini Kenya yameonyesha kuwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii zina ‘athari zinazoenea’ zaidi kwa jamii zilizo hatarini kuliko mbinu za kawaida za kuhamisha pesa. Mradi huu unalenga kuwafikia watumiaji 320,000 katika miaka miwili ijayo, watu hao wote wanaishi chini ya mstari wa umaskini.

Ubunifu na masuala mapya ya kutafitiwa

Kuibuka kwa teknolojia bunifu za utoaji wa misaada huibua masuala mapya kuhusu jinsi mifumo hii inavyofanya kazi, ikiwa inatimiza malengo ya waliyoibuni, ikiwa inakubalika na ina faida kwa jamii zinazoitumia. Kwa sababu Sarafu Zinazoshirikisha Jamii bado zinajaribiwa, kuna haja ya kuuliza maswali haya na kukusanya data zaidi ili isaidie katika kufanya uamuzi unaohusu mabadiliko yanayoendelea na utumiaji wa teknolojia hiyo. Mitazamo ya walengwa inapaswa kuzingatiwa hapa: watu wanachukuliaje Sarafu Zinazoshirikisha Jamii na wanazilinganishaje na kutumiwa pesa kidijitali au kusambaziwa vyakula au wa vitu visivyo chakula? Kwa upana zaidi, ingawa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii hupunguza chaguo walizo nazo walengwa za jinsi wanavyoweza kutumia rasilimali hizi (ikilinganishwa na pesa taslimu) hili limekusudiwa kuweka rasilimali zaidi ndani ya jamii na hivyo kuzalisha faida pana za kiuchumi. Je, walengwa wanaelewa na kuchukulia mifumo hii kwa namna hii? Pia kuna swali kuhusu jinsi teknolojia hii mpya inavyoingiliana na  mikakati iliyopo katika shughuli za kuishi na za kiuchumi ndani na karibu na kambi za wakimbizi – hasa katika makazi makubwa na ya muda mrefu.

Isitoshe, blockchain kwa jinsi zilivyo huzalisha rekodi za umma za miamala. Rekodi hizi zinaweza kuwa muhimu kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu ili kuongeza uwajibikaji/uwazi kwa wahisani na kupata data ambayo inaweza kuisaidia kuboresha mikakati kwa minajili ya kuleta faida kubwa zaidi za kiuchumi kwa jamii. Lakini, walengwa wanaoneleaje kuhusu kuchagua kati ya ujumuishwaji wa kifedha na faragha? Je, wanaelewa jinsi data yao inavyohifadhiwa na kutumiwa, na wana maoni gani kuhusu hili?

Tunahisi kuwa Sarafu Zinazoshirikisha Jamii zina uwezo wa kusaidia kuleta uwiano bora kati ya changamoto hizi na kuleta faida ya kweli kwa jamii zilizotengwa kiuchumi. Ushirikiano zaidi kati ya watafiti wa kitaaluma (kama wale wanaohusika katika mtandao wetu wa Uchanganuzi wa Data na Haki za Kidijitali Afrika Mashariki) na mashirika ambayo ni wanaanzilishi wa uvumbuzi huu utakuwa muhimu katika kukusanya data kutoka kwenye miradi ya majaribio inayoendelea ili kuhakikisha kuwa kuna manufaa ya juu kabisa kwa watoa misaada na wapokeaji wa misaada, na kwamba hatari zinazoweza kutokea zinapunguzwa.

Rosemary Okello-Orlale ni Mkurugenzi wa Africa Media Hub katika Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha Strathmore (r.okello-orlale@strathmore.edu). Steve Kenei ni Mchanganuzi wa Data katika Kituo cha Kimataifa cha Masuala ya Kibinadamu/Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (kenei.steve@redcross.or.ke).

This blog post was translated from English into Kiswahili by Semantics Africa Limited (word@semanticsafrica.com).

Related Blogs