Network blog

Mashirika ya Kiuchumi Yasiyo Rasmi na Ugeuzo Data katika Afrika Mashariki

Na Daivi Rodima-Taylor na Michael Kimani, Novemba 2020. [The original English blog post is available here]

Vyama vya kusaidiana na vikundi vya kuweka akiba vimekuwa na nafasi muhimu katika jamii nyingi za Kiafrika.  Huku simu za mkononi na pesa kwa njia ya simu zikiendelea kuwa sehemu muhimu  katika maisha ya kila siku ya watu wengi Afrika Mashariki, juhudi kubwa zinaendelea kufanywa ili kutumia programu mpya za simu na kompyuta pamoja na ushirikiano mpya na sekta rasmi ya kifedha kwa minajili ya kusimamia vikundi kama hivyo. Teknolojia mpya zinaonekana kutoa fursa bora za uwekaji rekodi kidijitali na ubadilishanaji habari kati ya washiriki wa vikundi bila kujali umbali waliopo. Hili ni muhimu hasa ukizingatia janga la COVID-19. Kwa upande mwingine, teknolojia hizi pia zinaweza kusababisha kuongezeka kwa urasimishaji wa vikundi, pamoja na uvunaji wa data, hali ambazo kimsingi zinaweza kufaidi kampuni za teknolojia na mashirika rasmi ya kifedha.

Tunajadili kwamba mwingiliano wa vikundi vya kiuchumi visivyo rasmi na teknolojia dijitali barani Afrika unaweza kufichua mabadiliko muhimu ambayo yanafanyika katika maisha ya watu na ushiriki wa raia katika muktadha wa ‘ugeuzo data’ unaoendelea – yaani michakato ambapo shughuli za kila siku za watu hugeuzwa kuwa vipande vya kidijitali vinavyoweza kuhesabiwa, kufuatiliwa na kusimamiwa na alogaridhimu. Makala haya ya blogu yanachunguza jinsi vikundi vya kusaidiana au ‘visivyo rasmi’ vya kiuchumu vilivyokita mizizi kihistoria na kitamaduni Afrika Mashariki, pamoja na kuongezeka kwa kujihusisha kwa vikundi hivyo na teknolojia dijitali. Tunauliza maswali kadhaa yanayoibuka kuhusu athari za mchakato huu katika maisha ya watu, uwezo wao wa kujiamulia kama watu binafsi na vikundi visivyo rasmi, michakato ya uratibu na ujumuishaji ndani ya vikundi hivyo. Makala haya ya blogu yanatokana na utafiti wa nyanjani uliofanyika Afrika Mashariki pamoja na mapitio ya maandiko ya wasomi na tasnia.

Kuelewa historia na muktadha wa kijamii wa vikundi vya kiuchumi

Katika jamii nyingi za Kiafrika, vikundi visivyo rasmi vimekuwa na jukumu muhimu katika kuunganisha riziki za wenyeji, pamoja na kusambaza rasilimali mpya kwa njia zinazokubalika kijamii. Kwa mfano, miongoni mwa jamii ya Wakuria wanaoishi kaskazini mashariki mwa Tanzania, vikundi kama hivyo viliibuka miaka mingi iliyopita kwa lengo la kushirikiana katika kazi za kilimo – kuna rekodi za kuwepo kwa vikundi hivyo nyakati za ukoloni katika nusu ya kwanza ya karne ya 20.  Ingawa kuongezeka kwa kilimo cha mazao ya biashara na vyama vya ushirika vya mauzo katika Tanzania ya baada ya uhuru kulifanya pesa kuwa jambo la msingi katika maisha ya wanavijiji, vikundi hivyo katika jamii ya Wakuria vilikuwa daraja muhimu katika uchumi mpya wa pesa hasa baada ya marekebisho ya kimfumo yaliyofanyika miaka ya 1980. Vikundi vya kusaidiana viliongezeka katika maeneo ya Wakuria – na vivyo hivyo katika mikoa mingine ya Tanzania – katika kipindi cha baada ya ujamaa. Vikundi vya sasa miongoni mwa jamii ya Wakuria hufanya shughuli za kilimo na zisizo za kilimo, kama vile useremala, kutengeneza matofali, ushonaji na kazi nyingine za mikono. Washiriki wa vikundi wanaweza kuendesha biashara, duka au shamba dogo la kilimo pamoja. Mara nyingi vikundi hivyo hujumuisha mizunguko ya kuweka akiba na kutoa mikopo na vinaweza kuwa na hazina ndogo ya kikundi ili kutoa msaada wakati wa dharura na vilevile kuwekeza ili wapate faida.

Mkutano wa kikundi kisicho rasmi cha kuweka akiba, Mkoa wa Mara, Tanzania. Picha: D. Rodima-Taylor

Hapo awali, vikundi vilivyo katika jamii ya Wakuria vilikuwa havikutani mara kwa mara na vilifanya kazi kama sehemu ya mtandao mpana wa ukoo au mbari. Vikundi vya kisasa vya jamii ya Wakuria ni vya kudumu zaidi na vina ngazi za madaraka na kanuni zilizobainishwa waziwazi. Licha ya vikundi hivi kuwa na muundo wenye ngazi za madaraka, mifumo inayozingatia makubaliano bado inatawala katika mchakato wa kufanya uamuzi katika vikundi hivi. Vivyo hivyo, umuhimu wa majadiliano kwa mdomo yaliyopewa kipaumbele juu ya hati zilizoandikwa umeshuhudiwa katika vikundi vinavyojisimamia vya chama nchini Kenya.

Kuongezeka kwa vikundi vya kusaidiana nchini Tanzania kunaweza kuhusishwa na kupungua kwa ajira katika sekta rasmi na kudidimia kwa vyama vya ushirika vya kilimo vya serikali katika kipindi cha baada ya ujamaa. ivi karibuni,vikundi vya kisasa vya chama nchini Kenya pia vimeshuhudiwa kuongezeka katika kipindi cha mageuzi ya uchumi huria ya miaka ya tisini. Vikundi hivyo vinatimiza majukumu mengi, yakiwemo ya kijamii na ya kiuchumi na vimeenea katika shughuli za fani mbalimbali, vikiwemo miongoni mwa wafanyabiashara masokoni na hata madereva wa  Uber katika uchumi unaozidi kupanuka wa wafanyakazi huria wa muda mfupi. Baadhi ya vikundi vimeibuka kuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha harakati za uraia miongoni mwa wafanyakazi wa kipato cha chini au walio katika sekta isiyo rasmi kama vile wanaoendesha matatu au bodaboda. Aghalabu, watu huwa katika zaidi ya chama kimoja, shughuli na faida zikiwa tofautitofauti.

Kuongezeka kwa uwezo wa kupata simu za mkononi na mtandao wa inteneti kwa njia ya simu Afrika Mashariki kumechochea vikundi vya chama kutegemea hata zaidi huduma za kifedha kupitia simu na njia za mawasiliano dijitali. Hali hii pia imehimiza sekta za fedha na mawasiliano kuchunguza teknolojia za kidijitali kwa ajili ya usimamizi wa vikundi na kuunganisha vikundi hivyo na huduma za sekta rasmi ya benki. Vifurushi vya programu za usimamizi digitali wa vikundi vinatengenezwa na kampuni za pesa kwa njia ya simu pamoja na zile za kutuma pesa kwa lengo la kuimarisha hatua za mwisho zinazohitajika kuwafikia walengwa wengi zaidi. Pia zinatengenezwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mashirika Madogo ya Kifedha pamoja na sekta rasmi ya benki inayojitahidi kupanua huduma zake ili kufikia jamii zenye kipato cha chini.

Kufanya vikundi vya chama viwe dijitali – mifano linganishi

Nchini Kenya, huduma kadhaa dijitali zimeibuka kwa ajili ya usimamizi wa vikundi vya kusaidiana.  ChamaSoft ni programu inayowezesha vikundi kuweka rekodi zao za hesabu kwa njia dijitali. Programu hii hutoa ankara za wanachama kiotomatiki, hudumisha taarifa za akaunti, huwakumbusha wanachama kulipa na kufuatilia historia ya miamala ya wanachama katika kikundi.  EazzyChama ni programu ya wavuti inayomilikiwa na Benki ya Equity ambayo inatoa njia ya kiotomatiki ya kuweka hesabu, kutoa ankara kwa wanachama na kusimamia mawasiliano kwa vikundi vya chama, hivyo kuvipa jukwaa dijitali la kusimamia mikopo ya ndani. M-Chama Account ni akaunti ya vikundi inayotolewa na Benki ya Shirika la Posta la Kenya (Postbank), inayohudumia vikundi vya chama vilivyosajiliwa na visivyosajiliwa. Wanachama wanaweza kuweka pesa na kuomba mikopo kwenye akaunti ya kikundi wakitumia simu zao za mkononi. Pia wanaweza kuweka pesa katika matawi ya Postbank na mawakala wa M-Pesa kote nchini.

Huduma za kidijitali ambazo zinajaribu kuiga muundo wa vikundi vya akiba vya tangu jadi pia zinaendelea kuongezeka katika maeneo mengine ya Afrika.  TigoPaare ni huduma ya akiba kwa vikundi kupitia simu za mkononi nchini Ghana. Huduma hii, ambayo inaiga utendaji wa vikundi vinavyojulikana kama  paare, inawawezesha wafanyabiashara wa mifugo nchini humo kukusanya rasilimali zao na kuratibu huduma za pamoja bila kujali umbali kati yao. Akiba ya kikundi iliyo kwenye akaunti za simu hupata riba ambayo hugawiwa wanakikundi, kadhalika jukwaa hilo husaidia kuunganisha vikundi na wafadhili pamoja na washirika wa nje, zikiwemo benki na Mashirika Yasiyo ya Serikali.

Vikundi vya stokvel nchini Afrika Kusini vilichimbuka katika karene ya 19.  Ingawa tangu jadi stokvel ni vikundi vya kuweka akiba ambayo inaweza kupatikana kwa mzunguko, katika Afrika Kusini ya leo, vikundi hivyo vinazidi kutumikia kuwekeza katika uchumi rasmi na vikundi vingi vina akaunti rasmi za benki. Chama cha Kitaifa cha Stokvel Afrika Kusini hufanya juhudi za kuratibu na kudhibiti vikundi hivyo. Kwa sasa chama hicho kinawakilisha zaidi ya Stokvel 800,000 zilizo na wanachama milioni 11 ambao hukusanya takribani Randi bilioni 50 kila mwaka. Programu kadhaa za simu za mkononi zimeibuka ambazo zinawezesha stokvel kudhibiti malipo na mawasiliano kati ya wanachama.  Stockfella inadhibiti takribani stokvel 2,000 zenye wanachama wapatao 14,000, ina leseni ya kuweka pesa na inafanya kazi kama mkopeshaji, huku ikitoa mikopo kwa vikundi vinavyotimiza vigezo. Programu nyingine ya simu mahiri inayoitwa Franc, inawezesha wanachama wa stokvel kuwekeza katika masoko ya fedha na hisa zinazoweza kubadilishwa.

Changamoto, fursa, mapungufu ya maarifa

Juhudi za kufanya shughuli za vikundi vya kusaidiana ziwe katika mfumo dijitali zimekabiliwa na changamoto nyingi. Jitihada za kutumia mifumo dijitali mara nyingi huendelezwa kwa mtazamo wa masilahi binafsi ya kampuni za teknolojia, kampuni za huduma za simu, benki na wahusika wengine wa kitaasisi. Mara nyingi, mahitaji hayazingatiwi sana.  Wakati huo huo, kuna utofauti mkubwa sana katika shughuli na kazi za vikundi vya chama, ambavyo vinahusisha shughuli na kazi za kijamii na kiuchumi, mbali na kuchanganya uwekaji akiba ya vikundi na miradi anuwai ya kilimo na isiyo ya kilimo. Kwa sababu hizo, vielelezo vinavyotolewa na programu kama hizo haviwezi kulingana na mahitaji ya vikundi. Muunganiko wa programu hizo na malipo kwa njia ya simu na chaguo la pesa taslimu mara kwa mara bado hautoshi. Vikundi vingi vya chama, hasa katika maeneo ya vijijini, bado ‘havina benki’ na wanachama wavyo wana uwezekano mdogo wa kutumia bidhaa zinazotegemea taasisi fulani za kibenki – kwa sababu ya ada, ukosefu wa hati rasmi za kujitambulisha, miongoni mwa sababu nyingine. Isitoshe, programu za vikundi dijitali mara nyingi zinalenga simu mahiri, ilhali simu za ‘kitochi’ au ‘kabambe’ zilizo na vipengele vichache ndizo nyingi miongoni mwa watu wenye kipato cha chini katika ukanda wa Afrika Mashariki. Isisahaulike kuwa mitazamo ya kampuni za teknolojia ya kifedha na ya vikundi vya kusaidiana kuhusu malengo, maadili na ufanisi wa shughuli za kikundi inaweza kutofautiana sana, huku vikundi vikiweka mkazo zaidi katika malengo ya kijamii kuliko viashiria vya ufanisi wa kifedha.

Kibanda cha huduma za pesa kwa simu katika soko kaskazini mwa Uganda. Picha: D. Rodima-Taylor

Kwa vile programu hunakili data inayozalishwa na vikundi vya chama, dukuduku kuhusu faragha zinaweza kuibuka. Kulinda taarifa za miamala ya washiriki wa vikundi ili isifikiwe na watu wa nje mara nyingi huonekana kuwa muhimu zaidi miongoni mwa wanavikundi kama hivyo. Shughuli za vikundi zinazowahusisha watu wenye hali sawa zinaweza kutoa nafasi salama kwa wanawake wasio na uwezo, mbali na kuwapa ulinzi dhidi ya mahitaji ya familia pana. Imani hiyo ya kuwa na faragha inaweza kudhoofishwa kwa sababu taarifa za miamala zinazidi kufikiwa na wahusika wengine, ambao hawajulikani kwa washiriki wa vikundi. Mahojiano ya hivi karibuni yaliyowahusisha wanavikundi vya  chama nchini Kenya yamethibitisha kuwa washiriki wa vikundi mara nyingi hawafahamu uwezekano wa wahusika wengine kupata taarifa zao kupitia programu dijitali pamoja na hatari ambayo hali hiyo inaweza kuletea faragha yao. Pia wana ufahamu mdogo sana wa haki zao za kulinda data yao ya kibinafsi, na wanaweza kukosa njia za kutumia haki hizo.

Athari ya mwelekeo dijitali wa vikundi vya chama  kwa ajili ya kuleta usawa katika ufikiaji wa kifedha na ushiriki wa raia walio wezeshwa bado hayajafahamika. Chama zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ufikiaji wa huduma za kifedha miongoni mwa watu wa kipato cha chini. Kwa vile vinatoa huduma bora mbadala za kuweka akiba na kupata mikopo vikilinganishwa na sekta rasmi, wakati mwingine vinaonekana kuwa tishio kwa taasisi zilizopo za kifedha. Kwa hivyo, upo uwezekano kwamba zana za kidijitali zinatengenezwa tu kama njia ya sekta rasmi ya kifedha kujumuisha na kudhibiti vikundi hivi?

Teknolojia dijitali zinaweza kurahisisha mtiririko wa pesa na taarifa, pamoja na kusaidia katika usimamizi wa vikundi kwa njia fulani. Wakati huo huo, utumiaji wa mifumo dijitali unaweza kuendeleza kutenganisha vikundi na mazingira ya kijamii. Kupitia programu za simu, vikundi vinaweza kuundwa na watu wasiojuana, mara nyingi lengo hubadilika kutoka akiba na ujasiriamali wa pamoja na kuwa uwekezaji wa kubahatisha faida. Hili linaweza kuwakosesha nafasi wale wasio na dhamana au mapato ya kutosha ya kuwawezesha kushiriki katika shughuli mpya, zinazoegemea sekta rasmi. Janga la COVID-19 pia limeleta changamoto zaidi katika mwingiliano wa ana kwa ana na mashauriano ya kutafuta makubaliano, shughuli ambazo ni muhimu sana katika uendeshaji wa chama . Badala ya kuwezesha vikundi, teknolojia dijitali zinaweza kuzuia uanuai na kujitosheleza kwavyo kwa kubuni huduma zinazolenga watumiaji wengi kwa pamoja, lengo kuu likiwa kujumuisha vikundi katika sekta rasmi.

Masuala ibuka ya kutafitiwa zaidi

Ili kuelewa utendaji, mabadiliko na uanuai wa vyama hivi vya hiari, lazima tuvitazame kwa kuzingatia historia yavyo kimaeneo na nafasi yavyo maalum ya kiuchumi, pamoja na mitandao iliyopo ya kijamii, miundo ya kijamaa na kanuni za kijinsia. Utafiti zaidi unahitajika haraka ili kuchunguza athari za programu dijitali katika mienendo ya watu kuhusiana na kuweka akiba, kukopa na ujasiriamali, na pia usawa wa kijinsia, haki za raia na ushiriki wao. Je, programu hizi zinavipa sauti vikundi, ambavyo ni watendaji huru, katika midahalo ya umma inayoendelea kuhusu kazi kwa haki na haki za wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi na kwenye uchumi unaokuwa haraka wa wafanyakazi huria wa muda mfupi? Je, zinatoa jukwaa linalowezesha ushiriki wa kisiasa na kiraia? Je, juhudi za kuendeleza mifumo dijitali zinatoa nafasi kwa harakati za mashinani na biashara zinazochipuka barani Afrika – au zinasaidia tu wahusika rasmi wa kifedha wa barani na kampuni za teknolojia za nje kujinufaisha kwa ruwaza za ushirikiano na mshikamano zinazopatikana barani Afrika? Kadri shughuli za vikundi vya kiuchumi zinavyozidi kugawanywa katika vipande vya kidijitali vinavyoweza kuhesabiwa na kufuatiliwa kupitia programu, ni nani atakayeweza kufikia data hii? Je, nani atafaidika na udhahiri mpya wa uchumi usio rasmi, na ni vipi washiriki wa vikundi wanaweza kudhibiti data yao wenyewe na kulinda faragha yao vizuri zaidi? Maswali haya na mengine mengi ya dharura yanahitaji majibu, ili kutathmini uwezekano wa unyonyaji au ukombozi unaotokana na mipango hii inayopanuka haraka ambayo inaleta vikundi vya kusaidiana vya Afrika Mashariki katika ulingo wa dijitali.  

Daivi Rodima-Taylor ni mmoja wa waratibu wa Mtandao wa Ugeuzo Data na Haki za Kidijitali ambaye pia ni mtafiti na mhadhiri katika Kituo cha Mafunzo ya Masuala ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Boston. Michael Kimani ni Mshauri wa Ubunifu na Mikakati ya Teknolojia ya Kifedha, Afrika Mashariki, na pia Mwanzilishi wa Cryptobaraza.

This blog post was translated from English into Kiswahili by Semantics Africa Limited (word@semanticsafrica.com).

Related Blogs